Monday, January 30, 2017

SAMSUNG YATHIBITISHA BETRI KUWA CHANZO CHA GALAXY NOTE 7 KULIPUKA, YAPATA HASARA YA DOLA 5.3 BILIONI



Kampuni ya kutengeneza bidhaa za kieletroniki ya Samsung imethibitisha kuwa betri ambazo zimetumika katika simu za Galaxy Note 7 zina kasoro na hivyo kusababisha simu kuwaka moto na kulipuka.
Katika taarifa ambayo imetolewa na kampuni hiyo ya Korea Kusini ilisema kuwa kuna uwezekano kuwa kukawa na tatizo lingine ambalo limesababisha lakini kwasasa wamegundua kuwa betri ndiyo chanzo.
 “Kwa hitimisho tu betri ndiyo limegundulika kuwa chanzo cha matukio ambayo yalitokea kwa Note 7,” ilisema sehemu ya taarifa ya Samsung.
Aidha Samsung imesema sababu ya tatizo kutokea katika betri ni uwezo mdogo wa kumudu matumizi ya simu hiyo jambo lililosababisha betri kuwa kupata joto kali na baadae kulipuka moto.
Pia kampuni hiyo imetangaza kuwa imepata hasara ya Dola 5.3 bilioni kwa ajili ya kurudisha simu hizo kiwandani ili kufanyiwa uchunguzi na kujua nini hasa chanzo cha simu hizo kuwaka moto na kulipuka.
Samsung wamesema kuwa kwa sasa wamejifunza na wana uhakika kuwa tatizo kama hilo halitajitokeza katika toleo linalofata la Galaxy Note 8 ambayo inataraji kutoka mwaka huu.
Simu ya Samsung Galaxy Note 7 ilitoka mwaka jana mwezi Agosti lakini baada ya mwezi mmoja simu hizo zilianza kuripotiwa kupata matatizo na hivyo Samsung ikarudisha simu zinazokadiriwa kufikia milioni 2.5 ili kuzichunguza.